Namna ya kutengeneza chachandu ya mboga kuepuka upotevu na uongeze kipato - SHAFIINAD

Breaking

TANGAZA NASI

test banner

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Sunday, 6 November 2016

Namna ya kutengeneza chachandu ya mboga kuepuka upotevu na uongeze kipato

Kwa hisani ya mkulima mbunifu naleta kwenu elimu juu ya kutengeneza chachandu
 
Msimu ambao mboga hasa za matunda kama vile nyanya na nyinginezo zinapokuwa nyingi, wakulima hupata hasara kubwa sana inayotokana na mazao hayo kuharibika haraka kutokana na uhaba wa soko.

Uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali nchini Tanzania, na kwingineko, umeshika kasi sana kutokana na jitihada zinazofanywa na wakulima katika kuongeza uzalishaji huo.
Hili ni jambo muhimu sana kwa kuwa walaji wanatoshelezwa bila kupata taabu, huku wakulima nao wakipiga hatua kadhaa za kimaendeleo.
Juhudi hizi zinakatishwa tama na ukosefu wa soko la haraka la mboga mboga na matunda, huku wakulima wakiwa hawana namna ya kuhifadhi mazao hayo kwa lengo la kusubiri soko au kwa matumizi ya baadae. Wakulima huacha mazao hayo yakioza ovyo, na baada ya kuoza wakulima wanakata tamaa kwa kuwa hupata hasara kubwa kutokana na upotevu huo.
Ni muhimu kwa wakulima na Wajasiriamali kufahamu namna mbalimbali wanavyoweza kuhifadhi na kusindika mazao wanayozalisha, ili wasiingie katika hasara isiyokuwa ya lazima.

Kwa kufahamu hilo, kikundi cha kina mama cha Tumaini kutoka King’ori wilayani Arumeru, wameanzisha jitihada za kuwakomboa wakulima wa mboga za matunda kama vile nyanya, vitunguu na hoho kwa kuanzisha utengenezaji na usindikaji wa chachandu (Appetizers).

Kupitia kikundi hiki, unaweza kufahamu namna ya kutengeneza chachandu ya vitunguu, nyanya, usindikaji wa maharagwe mabichi, jamu ya embe na karakara ikiwa ni hatua zote zitakazotakiwa hadi kufika sokoni.

1.    Chachandu ya Nyanya (Stewed tomato)

Hii ni aina ya kiungo ambacho hutumika kuongeza ladha kwenye chakula, pamoja na hamu ya kula.


IMG_0457
Namna ya kusindika chachandu ya nyanya

Dondoo: Kiwango cha mahitaji yatakayoainishwa hapo chini na maelezo yake ni kwa ajili ya kutengeneza na kupata kiasi cha chupa 12 za nusu (½) lita.

Mahitaji

• Nyanya sadoline 2
• Pilipili hoho kilo 2
• Vitunguu maji kilo 1¼
• Chumvi vijiko 2 vya chai

Namna ya kuandaa

• Osha nyanya na pilipili hoho vizu kwa maji safi
• Menya vitunguu vizuri
• Katakata vyote kwa muundo wa viboksi vidogo vidogo
• Weka kwenye sufuria
• Bandika jikoni
• Koroga taratibu kwa muda wa nusu saa ili mchanganyiko huo usiungue

Ufungashaji

• Wakati mchanganyiko ukiendelea kuiva jikoni, hakikisha unaandaa vifungashio/chupa
• Ni muhimu kuhakikisha kuwa chupa hizo zimeoshwa vizuri na kuwekwa kwenye chombo maalumu cha kuulia vimelea (Sterilizer)
• Weka mchanganyiko wa chachandu kwenye vifungashio kulingana na ujazo unaohitaji ukiwa bado wa moto
• Funga chupa/kifungashio kiasi
• Rudisha kwenye chombo maalumu cha kuulia vimelea
• Acha humo kwa muda wa dakika tano
• Ondoa na ufunge vizuri
• Pindua chupa/kifungashio mfuniko ukae chini. Hii itasaidia mfuniko kufunga vizuri
• Weka nembo tayari kwa mauzo

*Inashauriwa kuanza kuuza bidhaa hiyo baada ya wiki moja tangu siku ilipotengenezwa. Bidhaa hii inaweza kuwa salama kwa matumizi ya binadamu kwa kipindi cha miaka 2 tangu ilipotengenezwa.

Soko

Bidhaa hii inauzwa na kutumiwa na watu wa kada mbalimbali. Inaweza kuuzwa katika hoteli za kawaida na zile za kitalii, pamoja na maduka ya kawaida ya vyakula vya binadamu.

2.   Jamu ya embe na Karakara

Hii ni aina ya jamu ya asili ambayo inaweza kutumiwa kwa kula na mkate au aina nyinginezo za vitafunwa, au
mtumiaji anavyopendelea IMG_0460
kuitumia. Jamu hii inatengenezwa kutokana na mchanganyiko wa aina mbili za matunda, embe na karakara (Passion fruits)

Namna ya kusindika jamu ya embe na karakara

Dondoo: Kiwango cha mahitaji yatakayoainishwa hapo chini na maelezo yake ni kwa ajili ya, kutengeneza na kupata kiasi cha chupa 15 za nusu (½) lita.

Mahitaji

• Maembe 50 makubwa yaliyoiva vizuri
• Karakara ½ kilo
• Sukari nyeupe kilo 3
• Juisi ya limao lita ⅛


Namna ya kuandaa

• Osha maembe vizuri kwa maji safi
• Menya kwa uangalifu
• Katakata vipande vidogo vidogo
• Unaweza kusaga maembe hayo endapo si laini
• Osha karakara (passion fruits) vizuzi kwa maji safi
• Kata na utoe sehemu ya ndani (chakula)
• Changanya na maembe uliyokwisha kuandaa
• Weka sukari nyeupe kilo tatu kwenye mchanganyiko huo
• Weka lita 1 ya juisi ya limao
• Bandika jikoni
• Koroga taratibu kwa muda wa nusu saa
• Epua na ufungashe

Ufungashaji

• Wakati mchanganyiko ukiendelea kuiva jikoni, hakikisha unaandaa vifungashio/chupa
• Ni muhimu kuhakikisha kuwa chupa hizo zimeoshwa vizuri na kuwekwa kwenye chombo maalumu cha kuulia vimelea (Sterilizer)
• Weka jamu yako kwenye vifungashio kulingana na ujazo unaohitaji ikiwa bado ya moto
• Funga chupa/kifungashio kiasi
• Rudisha kwenye chombo maalumu cha kuulia vimelea
• Acha humo kwa muda wa dakika tano
• Ondoa na ufunge vizuri
• Pindua chupa/kifungashio mfuniko ukae chini. Hii itasaidia mfuniko kufunga vizuri
• Weka nembo tayari kwa mauzo

3.     Chachandu ya vitunguu (Onion mamaled)

Hii ni aina ya chachandu inayosindikwa kutokana na vitunguu. Chachandu hii ni kwa ajili ya kuongeza ladha kwenye chakula, pamoja na kuongeza hamu ya kula kwa watu wenye matatizo ya hamu ya kula.

Dondoo: Kiwango cha mahitaji yatakayoainishwa hapo chini na maelezo yake ni kwa ajili ya, kutengeneza na kupata kiasi cha chupa 12 za ujazo wa nusu (½) lita.

Mahitaji

• Vitunguu maji kilo 5
• Vinega lita 3
• Sukari kilo 3
• Karawei kijiko 1 cha chai
• Karafuu, punje 12
• Chumvi vijiko 10 vya chakula

Maandalizi

• Menya vitunguu kuondoa maganda
• Osha kwa maji safi
• Katakata kwa muundo wa viboksi vidogo vidogo
• Andaa sufuria safi
• Weka vitunguu kisha uchanganye na chumvi
• Funika kwa muda wa saa moja
• Osha vitunguu hivyo kwa maji safi ya baridi mara tatu
• Chuja ili kuondoa maji yote

Kutengeneza

• Bandika sufuria jikoni
• Weka vitunguu ulivyokwisha kuosha
• Weka lita 3 za vinega
• Changanya sukari kilo 3
• Weka karawei kijiko kimoja cha chakula
• Weka punje 12 za karafuu ulizokuwa umeandaa
• Koroga taratibu ikiwa jikoni kwa muda wa saa 3 bila kuacha

Kufungasha

• Weka kwenye vifungashio ikiwa bado ya moto
• Funga vifuniko kiasi
• Tumbukiza kwenye chombo maalumu cha kuulia vimelea chenye maji ya moto kwa muda wa dakika 5
• Ondoa kisha ufunge vizuri
• Weka lebo tayari kwa kuuza

*Baada ya matengenezo inashauriwa kupelekwa sokoni baada ya wiki moja.

Mamaled ya vitunguu inaweza kuliwa na chakula cha aina yoyote ili kuongeza ladha au hamu ya kula.

4.     Chachandu ya pilipili

IMG_0454Hii ni aina ya chachandu ambayo ni maarufu sana katika maeneo mengi ya chakula, ingawa utengenezaji na ubora wake hutofautiana kutoka mtengenezaji mmoja kwenda mwingine.

Aina hii ya chachandu itakayoelezwa hapa ni tofauti sana na chachandu nyingine za pilipili ambazo tumekuwa tukiziona. Hii ni kwasababu inazalishwa kutokana na pilipili ambazo zimezalishwa wa njia ya asili (organically) na inadumu kwa muda mrefu sana bila kuharibika tangu kutengenezwa na hata baada ya kuanza kutumika.

Mahitaji

• Pilipili kali kilo 5
• Pilipili hoho nyekundu 3
• Pilipili hoho za kijani 3
• Sukari kilo 3
• Juisi ya machungwa lita 1
• Vinega lita 1½
• Maji safi na salama lita 2

Maandalizi na matengenezo

• Osha pilipili kali na kuzikata kata kwenye vipande vidogo vidogo
• Osha pilipili hoho na ukate kwa pamoja
• Bandika kiasi cha maji lita 2 jikoni
• Weka mchanganyiko wa pilipili
• Koroga mpaka zilainike
• Epua baada ya kuiva
• Mimina kwenye mfuko maalumu wa kuchujia
• Ning’iniza juu ili maji yachuruzikie kwenye chombo kwa muda wa siku 1
• Kamua mabaki baada ya siku 1
• Pima maji yaliyochuruzika kufahamu kiwango kilichopatikana

Kutengeneza

• Baada ya kupima bandika jikoni
• Weka vinega kiasi cha lita 1½
• Weka sukari kilo 3
• Weka citric acid kijiko kimoja cha chai ili kuzuia kuharibika
• Koroga kwa muda wa saa 3 bila kuacha
• Weka kwenye sahani kuona kama iko tayari (Endapo iko tayari utaona mng’ao wake na haitashikana na sahani)
• Kama iko tayari weka kwenye vifungashio
• Funga kiasi
• Tumbukiza kwenye maji ya moto kwa muda wa dakika 5
• Ondoa kwenye maji ya moto na ufunge sawa sawa
• Weka nembo tayari kwa kuuza baada ya wiki moja
Makala hii imeandaliwa kutoka katika organization ya mkulima mbunifiu

No comments:

Post a Comment

Nitafurahi sana kama utaweka comment yako hapa chini kwa njia rahisi chagua ANONYMOUS wakati wa kuandika jina ili iwe rahisi we ku comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here