Kutengeneza na Faida za kutumia mbolea mboji - SHAFIINAD

Breaking

TANGAZA NASI

test banner

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Sunday, 6 November 2016

Kutengeneza na Faida za kutumia mbolea mboji 
Unaweza kupata matokeo mazuri kwa kutumia mbolea za asili katika kurutubisha udongo.

Kuna faida nyingi zinazotokana na matumizi ya mbolea za asili kama mboji na nyinginezo. Mbolea asili hutokana na kuoza kwa vitu vyenye uhai kama vile majani, miti na mabaki ya vyakula. Vitu hivi vinapooza hugeuka na kutengeneza virutubisho ambavyo husaidia
kurutubisha udongo na kupunguza gharama kwa mkulima kwa kuwa vitu vinavvyotumika ni vya asili.Mboji ikichanganywa kwenye udongo huifanya mimea kustawi na kuwa na afya ya kujikinga na magonjwa yanayoshambulia mimea. Kwa kawaida wadudu waharibifu hutafuta mimea ambayo ni dhaifu. 
Udongo ambao umeimarishwa kwa mboji huwa na mimea michache dhaifu. Kwa hivyo, siyo rahisi kushambuliwa na wadudu.Madini yaliyomo kwenye mboji husaidia kuyeyusha madini mengine yaliyo kwenye udongo na kufanya yapatikane zaidi kwa ajili ya mimea kwa muda mrefu. Vijidudu ambavyo hujilisha kwa njia ya mbolea ya asili kwa muda mfupi hushikilia udongo pamoja, na kuufanya udongo uwe bora na wenye afya.Utumiaji wa mboji huondoa utumiaji wa mbolea za chumvichumvi na dawa za kuua wadudu ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa afya za watu na udongo, ambazo pia ni gharama sana kununua.Mahitaji Ili kutengeneza mboji unahitajika kuwa na malighafi za kijani na kahawia. 
Mimea yenye kijani kibichi na ambayo haijachanua inafaa zaidi katika kutengezeza mboji, na iwe imekatwa karibuni. Mabaki ya chakula na matunda pia yanajumuishwa katika kundi la malighafi za kijani.Kundi la malighafi za kahawia ni pamoja na mimea ambayo imekauka baada ya kukatwa muda mrefu, pamoja na kinyesi cha wanyama wafugwao. Udongo na maji ni sehemu muhimu ya mahitaji kwa ajili ya kutengeneza mboji.Ili uweze kutengeneza mboji nzuri, unatakiwa kurundika rundo kwa  matabaka. Kiwango cha wastani kinachofaa kutengeneza mboji ni chenye urefu wa mita moja, na mita moja upana. Rundo ambalo ni dogo kuliko hili haliwezi kuhifadhi joto la kutosha kuozesha malighafi.

Hakuna kikomo cha ukubwa wa biwi la mboji, inategemea na ukubwa wa eneo ulilonalo na unataka mboji kiasi gani.Vitu visivyotakiwaMabaki ya mimea ambayo imeambukizwa magonjwa au imeshambuliwa na wadudu haitumiwi kwani inaweza ,kuwa na mayai ya wadudu na inaweza kuendelea kuzaliana.Pia mimea yenye tindi kali kama
vile migunga na Eucalyptus haifai, ijapokuwa kuna wakati inaweza kutumika kutengeneza mboji maalum kwa ajili ya kuongeza kiwango cha tindi kali kwenye udongo inapohitajika.  Halikadhalika magugu sugu kama sangare, mashona nguo na ukoka mgumu hayafai kwa kuwa yatasambaza mbegu za magugu katika shamba lako.Usitumie kinyesi cha wanyama kama mbwa na paka.Kutengeza mboji Ondoa majani yote pamoja na vitu vingine vinavyoweza kuharibu mboji yako, kisha lainisha udongo kiasi cha inchi sita kwa kutumia rato au jembe. Hatua hii inasaidia maji kupenya chini ya rundo la mkusanyiko wa kutengenezea mboji.

•Tabaka la kwanza linatakiwa kuwa kubwa kuliko matabaka mengine. Unaweza kutumia majani makavu, mabuwa ya mahindi na matawi madogo madogo ya miti. Vitu hivi pia ni vizuri kwa rundo la mboji na hurahisisha umwagiliaji maji. Weka rundo la tabaka la kwanza la mabuwa ya mahindi vijiti na matawi madogo madogo ili liwe tabaka lenye inchi sita
kwa mita moja kila upande.

• Tabaka la pili liwe na ukubwa wa inchi mbili na malighafi za kijani. Kumbuka kwamba: Tabaka liwe jembamba kuliko tabaka la kwanza. Kama una mabaki ya chakula ongeza kwenye tabaka hili.

•Tabaka la tatu ni tabaka la udongo lililochanganywa na mbolea au majivu. Tabaka hili liwe jembamba, kama unene wa robo inchi.
Unahitaji kutumia kiasi kidogo tu cha mbolea  kufunika sehemu ndogo tu katikati ya rundo la mboji kama vile futi moja kwa futi moja. Ni muhimu kutotumia mbolea nyingi kwenye rundo la katikati. Kama unatumia majivu, kiasi  kidogo tu kitumiwe katikati ya rundo la mboji. Ukishaweka mbolea katikati, unaweza kuizungushia udongo kufunika tabaka la kwanza.Wakati wote unahitaji kuongeza maji  ya kutosha kwenye rundo la mboji ili liwe na unyevunyevu, lakini yasiwe mengi kiasi cha kutota. Kumbuka, rundo la mboji liwe na unyevunyevu mfano wa sponji iliyowekwa kwenye  maji na kukamuliwa.Hivi ndivyo inavyotakiwa, na kama unataka kuongeza matabaka, rudia kama ulivyofanya mwanzo. Tabaka la majani makavu, ya rangi ya kahawia lenye inchi mbili, likifuatiwa na tabaka la kijani la inchi mbili, likifuatiwa na tabaka jembamba la udongo uliochanganywa na mbolea au majivu au vyote. Endelea kuweka matabaka haya mpaka matabaka yako yawe na urefu wa futi tatu au nne kwenda juu.Tabaka la juu na la mwisho liwe la majani makavu ya kikahawia lenye  unene wa inchi tatu. Hii husaidia kuhifadhi harufu ambayo wakati mwingine hutokea wakati wa uozaji. Hii pia husaidia kufukuza wanyama ambao huvutiwa na kutaka kuona kuna nini kwenye rundo la mboji.

Matumizi

Rundo la mboji litakapokuwa tayari, utabakiwa na mboji ambayo itaonekana kama udongo mweusi ulio na mbolea nzuri. Tandaza tabaka jembamba kwenye mazao yako na mimea  itastawi na kunawiri vizuri.

Angalizo

Biwi la kutengenezea mboji liwe karibu na mahali ambapo mbolea hiyo itatumiwa ili kuondoa gharama za usafiri.Ni vyema kufikiria juu ya wanyama na wadudu wanaoweza kuvutiwa na biwi la mbolea, mfano nyoka na panya. Hakikisha kuwa biwi la kutengenezea mboji linakuwa mbali na nyumba.

No comments:

Post a Comment

Nitafurahi sana kama utaweka comment yako hapa chini kwa njia rahisi chagua ANONYMOUS wakati wa kuandika jina ili iwe rahisi we ku comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here